cover

MAMBO YA MUHIMU KUJUA KWA HABARI YA KUFUFUKA KWA BWANA YESU

Mwl. Christoher Mwakasege • KKKT • Lutheran • 2026-01-18
ScripturesMathayo 28:1 – 7

SOMO NA MWL. CHRISTOPHER MWAKASEGE Bwana Yesu asifiwe milele. Naamini unaendelea vizuri, kwa msaada wa Mungu aliye hai, katika jina la Yesu Kristo. Ndani ya somo lililotangulia, tulijifunza maana ya 1, ya maneno ambayo Mungu alinijulisha ya kwamba ameamua kusema na watu wanaopitia katika majaribu. Mungu anasema: “Siku ya tatu ya jaribu lako imefika”. Maana ya 1 ya maneno haya nilikwambia ni hii: “Siku ya tatu ya jaribu lako ni siku ya kufufuliwa kwa matumaini yako”. Maana ya 2 ya maneno haya, ninayotaka kukufundisha leo ni hii: “Siku ya tatu ya jaribu lako, ni siku ya kuondolewa kwa mazuio ya kimfumo, yanayokuzuia usitoke katika majaribu yako yaliyokusonga” Mambo matatu nataka nikushirikishe katika maana hii ya 2, yanayohusu siku ya tatu aliyofufuka Yesu Kristo. Jambo la 1: Mazuio ya kimfumo yanayokuzuia usitoke katika majaribu yako, yanalenga kuzuia isijulikane ya kuwa Yesu amefufuka, na yu hai milele na milele. Kwa hiyo, unapoona majaribu ya kimfumo yanakulenga wewe, ujue hayakulengi wewe, bali yanalenga kukuzuia usije ukatumika au usije ukaendelea kutumika kuthibitisha ya kuwa Yesu amefufuka, na yu hai pia ndani ya mifumo hiyo! Sababu ya kwanza; ya mazuio ya kimfumo kutengeneza mazingira ya jaribu kuwa gumu, ni kwa nia ya kutafuta kuzuia ufufuo wa Yesu usidhihirike, na usijulikane, na usikubalike. Mifumo yoyote inaweza kutumika katika hili – kwa mfano: mifumo ya kiofisi, au mifumo ya kidini, au mifumo ya kisheria; au mifumo ya kifamilia, au mifumo ya kieneo, au mifumo ya kiutawala – nakadhalika. Nia ya mazuio hayo ni kuua nguvu ya imani, isitumike katika kumtegemea na kumtumaini Mungu, katika kufanikiwa kwa mtu ndani ya mifumo. Hii ni kwa sababu biblia inasema hivi: “Na kama Kristo hakufufuka, imani yenu ni bure…” (1 Wakorintho 15:17). Kwa hiyo Imani, ikifanya kazi kukusaidia kazini au katika maisha, ni udhihirisho tosha unaothibitisha kuwa Yesu amefufuka! Unalipata hili na kulielewa? Sababu ya pili; kwa nini mifumo inaweza kutumika na shetani kukusonga na jaribu, ni ili usiendelee kuiamini mamlaka uliyonayo ndani ya Kristo aliyefufuka, uliyopewa siku ulipookoka. Mamlaka hiyo inakupa mamlaka juu ya mifumo mbalimbali. Biblia inatujulisha ya kwamba, tulipookoka Mungu “alituhuisha pamoja na Kristo; yaani tumeokolewa kwa neema. Akatufufua pamoja naye, akatuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho, katika Kristo Yesu” (Waefeso 2:5, 6). “…juu sana kuliko ufalme wote, na mamlaka, na nguvu, na usultani, na kila jina litajwalo, wala si ulimwenguni humu tu, bali katika ule ujao pia…” (Waefeso 1:21) Shetani asingetaka uijue mamlaka hii uliyopewa katika ulimwengu wa roho, ili usije ukaitumia kuweka nuru ya Mungu, na haki ya Mungu, na amani ya Mungu, na furaha ya Mungu, na mafanikio ya Mungu katika mifumo inayohusika na wewe. Kumbuka ya kuwa; jaribu unalokutana nalo katika mifumo, linalenga kuzuia kujulikana kwa nguvu za ufufuo wa Kristo, katika kukutumia wewe kufanikisha mifumo hiyo inayokuhusu. Kwa hiyo, usikate tamaa wala usife moyo, bali jipe moyo mkuu, ukijua ya kuwa mfumo wa ufalme wa mbinguni upo pamoja na wewe, ili ukushindie jaribu ulilokutana nalo katika mifumo inayokuhusu! Jambo la 2: Kumbuka ya kuwa ufufuo wa Yesu katika siku ile ya tatu, ulikuja kujibu kimatendo swali ulilonalo – la nani atakusaidia kuondoa zuio hilo la kimfumo katika mfumo unaokuhusu, ambalo limekuwa jaribu kubwa kwako, linalozuia matumaini ya kesho ya maisha yako. Wale wanawake watatu walioamua kwenda kaburini kwa Yesu, alfajiri ya siku ya tatu, walikuwa na swali hili: “Ni nani atakayetuvingirishia lile jiwe mlangoni pa kaburi?” (Marko 16:3). Wale wanawake walijua ya kuwa, ili wafanye walichotaka kufanya kwa ajili ya Yesu Kristo wakifika kaburini, ni budi wapate msaada wa kuvingirishiwa jiwe lililokuwa mlangoni pa kaburi. Lakini kutokujua ni nani wa kuvingirisha jiwe kwa niaba yao, kukageuka kuwa jaribu kwao. Na wewe – inawezekana upo hapo ulipo, na kuna jambo unalotaka kulifanya kwa ajili ya utukufu wa Kristo Yesu, lakini kuna zuio katika mfumo uliomo, ambalo limekuwa “jiwe” kwako. Na kumpata mtu wa kukusaidia kuliondoa, kumegeuka jaribu kwako! Wanawake wale watatu walijiuliza lile swali, kwa sababu “wakuu wa makuhani, na mafarisayo” na “Pilato”, walishirikiana kimifumo, ili kuweka mazuio manne ya kimfumo, ili kuzuia lisitimie wala kudhihirika neno alilosema Yesu ya kwamba: “Baada ya siku tatu nitafufuka” (Mathayo 27:62, 63). Mifumo ile, ikakubaliana kuweka mazuio manne, ili yawe majaribu yasiyovukika, ili yatumike kuzuia kufufuka kwa Yesu! Zuio (au jaribu) la 1: Waliondoa jiwe mlangoni mwa kaburi, lililowekwa na Yusufu wa Arimathaya (Marko 15:43 – 47); na badala yake wakaweka jiwe “kubwa mno” (Marko 16:4). Zuio (au jaribu) la 2: Walilitia “lile jiwe muhuri” (Mathayo 27:66), ili kuzuia kisheria jiwe (au jaribu) lisije likaondolewa bila kibali cha mwenye muhuri ulio juu ya jiwe. Zuio (au jaribu) la 3: Waliweka “askari walinzi” (Mathayo 27:66), pale kaburini, ili zuio (au jaribu) lile lilindwe kwa kutumia nguvu ikibidi, ili kuzuia kuondolewa kwa jiwe (au jaribu). Zuio (au jaribu) la 4: Walitengeneza uongo wa kimfumo, ili kutumia hongo ya fedha “kuwachafua wafuasi wa Yesu”, kwa lengo la kuona ya kuwa, ushuhuda wao wa Yesu kufufuka haukubaliki kwa watu watakaokuwa wanaambiwa ya kwamba Yesu amefufuka – na yu hai! (Mathayo 28:11 – 15). Jambo la 3: Yesu alipofufuka “…malaika wa Bwana alishuka kutoka mbinguni, akaja akalivingirisha lile jiwe akalikalia” (Mathayo 28:2). Wale wanawake walipofika kaburini wakakuta jiwe (au jaribu) limevingirishwa (Marko 16:4). Kilichotokea “Jiwe” lile lilipovingirishwa, ni kule kuondolewa kwa “mazuio yote” na “majaribu yote” yaliyokuwa yanategemea jiwe kuwepo kaburini! Ni maombi yangu kwa Mungu, kwamba imani yako isitindike, kwa sababu tu unakwamishwa na jiwe, au zuio, au jaribu, unalopitia katika mfumo unaokuhusu. Siku ya tatu ya jaribu lako imefika! Jaribu hilo limefika mwisho wake! Yesu amefufuka! Na jiwe (au jaribu) lililokuwa linakuzuia limeondolewa! Nakuombea ya kuwa, jiwe (au jaribu) ambalo limekuzuia kwa muda mrefu katika mfumo huo, Mungu aliondoe kwa nguvu ya ufufuo wa Yesu, na Mungu aligeuze hilo jiwe, liwe “kiti” chako cha kukalia, unapotoa ushuhuda wa jinsi Yesu aliyefufuka, alivyokusaidia na kukushindia! (Mathayo 28:1 – 7). Tuzidi kuombeana. Somo hili litaendelea.

Comments

No comments yet.

Please login to comment.