NAMNA YA KUENDEA MILKI ZAKO ULIZOAHIDIWA NA MUNGU NA ZILE ZILIZO KATIKA MIKONO YA ADUI.-DAY 1
ScripturesMwanzo 1:26
*SEMINA YA NENO LA MUNGU RGCM DODOMA*
*NAMNA YA KUENDEA MILKI ZAKO ULIZOAHIDIWA NA MUNGU NA ZILE ZILIZO KATIKA MIKONO YA ADUI.*
_*Na Ev, Daniely Joshuan.*_
*25th April 2024*
Leo naweka msingi na kesho nitaendelea na siku ya jumamosi itakuwa ni hatari. Na natangaza kwenye Anga la Dodoma hatari na kwenye maisha yako. Hatari hii si ya uharibifu bali ni ya kukuamisha na kukupeleka kwenye maisha mengine.
Mungu alipomuumba mwanadamu toka kwenye misingi ya ulimwengu alimuumba katika kanuni mbili katika usawa. Au nitumie kanuni hii, wewe kuwa mtu na kutofautishwa na wanyama au viumbe vingine, sababu ya Mungu kuumba mtu imefungamanishwa katika mambo mawili na ni kanuni.
Hauwezi kuwa mtu ambaye Mungu anamtazama chini ya jua kama hauna hizi kanuni mbili.
*Moja*
_*Ibada*_
Mwanadamu ameumba chini ya hii kanuni inayoitwa ibada. Kinachomtofautisha mwanadamu na viumbe vingine ni ukweIi wa mwanadamu kunyenyekea chini ya Mungu wake. Aliposema na tumfanye mtu kwa sura na kwa mfano wetu, moja kati ya vitu unavyotakiwa kujua ni tabia ipi ya Mungu ambayo anaifurahia utagundua ni ibada.
*Mwanzo 1:26*
_*Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi.*_
Hapa tunaweza kuona vitu vingi sana na ndiyo maana Yesu alipokuja wakati anafundisha sala ya Baba yetu. Na alipofundisha ile sala hakuwa anamaanisha watu waombe kwa kuirudia ile sala. Ubaya wa dini umetuonyesha hiyo ndo sala. Sasa Yesu alitupa maelekezo namna ya kuomba kwa wale waliosoma vyuo vikuu wanajua kitu kinaitwa COURSE OUTLINE . Na hii inatuonyesha kwamba unaweza kurudia sala hii na bado ukalogwa. Yesu alikuwa anawaonyesha funguo za namna ambavyo mtu anaweza kuomba.
Kwa mfano anavyosema Baba yetu...
Kama wewe ni msomi wa Biblia katika vitabu vya injili utaona kitabu cha Yohana kilikuwa kinamfunua sana Baba na mwana. Na Yesu alipotaka majibu ya haraka aliomba kwa kusema Baba. Angalia Yohana 11:41
_*Basi wakaliondoa lile jiwe. Yesu akainua macho yake juu, akasema, Baba, nakushukuru kwa kuwa umenisikia.*_
Kumbuka alipokuwa anawafundisha aliwaambia waanze kwa kusema Baba na hapa tunaona namna ambavyo anaomba na tunaelewa matokeo ya maombi haya. Vivyo hivyo aliomba wakati wa kuyakaribia mateso ya msalaba.
Kama wewe ni msomi wa Biblia unajua kwamba kila neno lina maana sana. Ni wazi kwamba kila Yesu alipotaka Baba atende alianza kwa jina la Baba.
Na alipomaliza alisema uliye mbinguni, hapo tumeanza kuona kwamba ukitaka majibu lazima uanze na neno Baba kwa kutambua UBABA WAKE. Sasa uliye mbinguni limetamkwa kwa kusudi kabisa. Ni muhimu kujua kwamba ni kitu gani kinaendelea mbinguni. Anaposema uliye mbinguni tunaelewa maandiko yanasema kwamba Mbingu ni kiti changu cha enzi, na dunia ni mahali pa kuweka miguu yangu; mtanijengea nyumba ya namna gani? Na mahali pangu pa kupumzikia ni mahali gani? *Isaya 66:1* Hapa sasa utarudi kwenye kile kitu ambacho kinaitwa ibada. Hivyo basi kile kinachomfanya mwanadamu mwanadamu ni kuabudu. Ukienda mbinguni sasa hizi utakutana na wazee wakisema Mtakatifu Mtakatifu.
*Pili*
_*Kutawala*_
Mungu alipoumba vitu vyote na akasema ameshaviumba viko vizuri je vitakaa chini ya mamlaka ya nani? Aliposema tumuumbe mtu alisema wakatawale samaki wa baharini na vyote vilivyoko chini ya jua viwe chini ya mikono yake. Mungu alipowaumba aliwaweka kwenye bustani ya Edeni na alipomaliza unaweza kuniuliza sasa mbona hakukuwa na ibada. MUNGU alimuambia mwanadamu vyote kula ila mti huu wa matunda ya kati usile, unaweza kuona namna ambavyo Mungu alimuwekea kanuni ya kutii. Utagundua kwamba kila ibada ina aina ya utii ndani yake. Na mwanadamu aliposhindwa kutii ndipo alitolewa kwenye kumiliki.
Mungu akamtengenezea mtu mfumo na ulikuwa ni mfumo wa ibada. Kila mfumo wa kuabudu una vitu vya kufanya na vitu ambavyo hautakiwi kufanya. Sasa utaelewa maisha yako ya ibada yanaonyesha maisha yako ya umiliki. Haya ndiyo yaliyotokea kwa maisha ya Baba zetu wakina Ibrahimu kwa kadri walivyozidi kuabudu ndivyo walizidi kumiliki.
Kumbuka haukuumbwa kumiliki watu bali kumiliki vitu. Dunia ni mbaya kwasababu watu wanatafuta kumiliki watu. Ndiyo maana ukiona kazi yako ni kupingana na watu, kuwanyamazisha jua kwamba haujajua kile ambacho kilikuleta duniani. Baba zetu wa kiimani walipokuwa wanafanya maisha yao ya ibada kama kitu walichoumbiwa sababu hiyo walimiliki.
*Mwanzo 13:2*
_*Naye Abramu alikuwa ni tajiri sana kwa mifugo, kwa fedha, na kwa dhahabu.*_
Kama ibada yako iko pungufu na vile unavyomiliki kuna shida mahali. Kuna watu ambao wanayatoa maisha yao kwa shetani na wengine tunawaona kwenye mitandao. Kwa kadri wanavyotoa maisha yao ya ibada ndivyo wanazidi sana kumiliki. Unajua kwanini watu wanajiunga kumuabudu shetani ni kwasababu wanataka kurudisha nguvu ya kumiliki.
Kanuni ni hii una abudu kisha unamiliki. Kuabudu ni sawa sawa na kumiliki. Ukichukua moja na ukaacha nyingine unapoteza mwendo wako.
Unajua Yesu alipokuja kwenywe maisha haya alikuja kufanya nini? Alikuja kurejesha vitu hivi viwili, kurejesha ibada na umiliki. Kwenye ufunuo anasema _*ukawafanya kuwa ufalme na makuhani kwa Mungu wetu; nao wanamiliki juu ya nchi.*_ *Ufunuo wa Yohana 5:10*
Kila unapokwenda kumbuka haya mambo mawili kwamba mimi ni mwanadamu ili niweze kufanya mambo mawili, kuabudu na kumiliki.
*Luka 4:5-6*
_*[5]Akampandisha juu, akamwonyesha milki zote za ulimwengu kwa dakika moja. [6]Ibilisi akamwambia, Nitakupa wewe enzi hii yote, na fahari yake, kwa kuwa imo mikononi mwangu, nami humpa ye yote kama nipendavyo.*_
Milki zote kwa dakika moja hii ilikuwa swala la kiroho. Maabudu unayoyatoa ndiyo uwezo wako wa kumiliki kama iko kinyume kuna swali hapo? Utagundua kwamba Yesu kuonyeshwa milki zote kwa dakika moja ilikuwa ni zaidi ya swala la kimwili.
Kumbuka kwamba kila jaribu ambalo Yesu alipitia lilikuwa linamuhusu asilimia 100%. Kumbuka kwamba hakuna jaribu ambalo linakuja ambalo halikuhusu likakuinua. Shetani aliona namna ambavyo Yesu alikuwa na umasikini na kuzaliwa katika hali hiyo hivyo shetani alijua kwamba kwa asilimia 100% Yesu angeshindwa.
Linakuwa jaribu tu kama umeshinda lakini kama haujashinda si jaribu. Na shetani anapokuja kwako haji kujaribu anakuwa na uhakika kwamba atashinda. Tunayaita haya majaribu ya Yesu kwasababu alishinda kama angeshindwa tusingeita majaribu bali anguko. Hivyo utaona kwamba shetani anapokuja kukujaribu aamini kushindwa na ndiyo maana hakati tamaa. Alimjaribu Yesu mara ya kwanza na aliposhinda alimpeleka kwenye kiwango kingine cha kumjaribu.
Tuangalie mambo saba ya haraka hapa.
*Jambo la kwanza*
_*Kupandishwa juu au kuchukuliwa juu*_
Ukitaka kupata miliki yeyote lazima ujiulize nani atakupeleka mahali pa juu ya kuona. Kuna miliki hauwezi kumiliki mapaka uende mahali pa juu kwenye kilele. Nani atakupeleka pale, shetani anaweza kukupeleka na ukaona, au ni rafiki zako au ni Mungu. Na watu wote watakaokupeleka pale watahitaji kuabudiwa.
Kwa maoni yangu usiruhusu shetani wa watu kukupeleka pale. Kuna watu kwenye maisha watataka kuabudiwa maana wanasema wao ndiyo waliokupeleka pale. Kuna aina ya umiliki hauweI kumiliki mpaka uwe na mtu utakayeamua akupeleke pale juu.
Wako watu waliopelekwa na waganga wa kienyeji, wako watu waliopelekwa na majini. Na wanapata shida sana maana wanashindwa kutoka huko. Swali langu kwako nani? Atakupeleka pale? Shetani anaweza kukupeleka na Mungu anaweza kukupeleka lakini watu wanaweza kukupeleka. Kuna mambo unawaza kwasababu haujapelekwa juu, unawaza kwenda kariakoo kufunga mzigo na kuuza Dodoma kwasababu haujapandishwa juu na kuona kuna china kuna Amerika.
*Jambo la pili*
_*Akamuonyesha*_
Nani atakusaidia kuona? Mungu anaweza kukuonyesha, shetani anaweza kukuonyesha na watu pia. Kuna watu wanaona kijijini kwasababu ya mahali walipo chini. Unajua miliki inafungamanishwa na kuona. Watu hawamiliki kwasababu hawaoni. Kuna watu hawaoni fursa na hawajui hata chakufanya. Shida si kwamba hakuna chakufanya shida ni kwamba huko chini, kuna mahali watu wanachukuliwa na kupelekwa juu na wakaona. Sina kazi, sina chakufanya, sina mtaji swali unaangalia kutokea wapi? Ukiwa sehemu tambarare utaona ambacho hautakiwi kuona.
Yesu hakuona kile ambacho shetani alitaka aone. Umesimamia wapi kunaamua unaona nini?
*Jambo la Tatu*
_*Mpaka juu*_
Kuna aina ya milki ambazo hauwezi kuona ni mpaka umepandishwa juu. Kuna mahali ukifika kihuduma unaona mbele. Unaweza kwenda na Mungu mpaka kileleni juu na ukaona miliki na unpofarakana na Mungu hautaona tena, na kile ambacho watu wengi wanafanya wanaanza kuwa wanyang'an'yi.
Ni hatari sana kupoteza kuonana kwako ikiwa mahali pa juu.
Ukiwa kwenye kilele lazima uwezo kuona mataifa. Ikiwa wewe ni mfanyabiashara lazima uweze kuona umekaa na mataifa. Umesimama wapi kutasababisha kuona unapoenda.
Umesimama wapi Binti uone uzao wako, kama hauna mahali uliposimama utaona wengine na kuwashangaa. Ukitaka kuona tafuta ni wapi umesimama. Mimi Mungu alikuwa ananionyesha nilipo wakati hakuna picha kabisa na wala hakuna fedha. Je unajiona wewe ujijihudhurisha mbele ya mataifa, mbele ya wakuu.
*Jambo la Nne*
_*Dakika moja*_
Siri ya milki haipo katika miaka ipo katika dakika. Wazo la dakika moja linaweza kukupeleka kwenye hatima . Siri ya milki haipo katika miaka. Shetani hakutumia miaka kumshawishi Yesu alitumia dakika moja. Unajua pia unaweza kupoteza milki yako kwa dakika moja. Watakuandalia mikataba hewa na utaweka sahihi ndani ya dakika moja utakuwa mtupu.
Usisahau tulipotoka wewe ni mtu kwasababu ya mambo mawili, kuabudu na kumiliki. Uwezo wako wa kumiliki unaenda sambamba na kuabudu kwako.
Swali langu kwako, unatumiaje dakika moja uliyonayo?
Haikuwa vyepesi Yesu kuona ulimwengu wote kwa dakika moja, hii ni siri.
*Jambo la Tano*
_*Ahadi za kumpa enzi na Fahari*_
Kumbuka kwamba kuna watu wametoa maisha yao kwa shetani na kwasababu hiyo wamemilikishwa. Ndiyo maana nilikuambia kuna watu ambao wamempa shetani maabudu na tunaona namna ambavyo wamekuwa na maisha ya kumiliki.
Unapoelewa siri utatolewa nyuma na kuwekwa mbele.
Shetani hana shida ya kuwapa watu kumiliki yeye anataka ibada tu kisha atakumilikisha.
*Jambo la Sita*
_*Vyote vimo mikononi mwangu*_
Unafikiri shetani alikuwa anadanganya kwamba viko mikononi mwake. Tupo mwisho wa miaka na vingi unavyoviona viko mikononi mwa shetani. Wewe kupata fedha ikakusaidia kujenga nyumba na ukatoa sadaka ni neema sana. Kile ambacho shetani anakifanya ni kuhakikisha anafanya maisha yako kuwa magumu sana, nani kukuonyesha kwamba kile unachoabudu kina faida gani? Ndipo hapo watakuja waijilisti wa kipepo kukuonyesha namna wao wamefanikiwa kule wanapoabudu kwa shetani. Hizi ni kanuni za kiroho hauwezi kukaa mahali ukabaki pale pale haiwezekani na miaka inaenda.
Adui ametawala mifumo ya kiuchumi, yuko tayari kahaba apate kazi na wewe ukose. Alipokuwa anasema vyote viko mikononi mwake si utani tangu Edeni mwanadamu aliposhindwa kuwa ibada ndipo alimyanganya miliki yake.
Je una ahadi za Mungu za kumiliki?
Wakristo wangejua kike mbacho neno limebeba kama ahadi gani wangelia. Maana kile Mungu ameahidi na namna watu walivyo ni vitu viwili tofauti. Walokole tunateseka, maisha ya shida. Unamuangalia mtu namna hii na anateseka kweli kweli lakini anampenda Mungu.
Shetani anajua kwa wewe kuwa ulivyo kuna wakati utamkana Mungu wako na kama sis wewe basi ndugu zako watauliza Mungu wake yuko wapi?.
Shetani anaweza kukuruhusu kuabudu lakini akakunyima milki zako anachowinda ni ibada bado. Kumbuka vitu hivi viwili vinaenda pamoja.
Wewe kupata nafasi ya kusoma ujumbe huu ni alama ya wazi kwamba Bwana anakurejesha kwenye milki zako..
*Jambo la Saba*
_*Humpa ye yote kama nipendavyo*_
Unaona watu ambao hawajaokoka wanakula vizuri kuliko wewe. Mwisho shetani anampa sharti Yesu kwamba akitaka ampe amsujudie. Shetani uwa natafuta nafasi moja tu kuabudiwa. Mkatae Yesu na niabudu mimi, vunja kanuni za kiroho na niabudu. Elewa kwamba kumuabudu shetani si swala la kumuinamia, wengine wanamuabudu kwa uzinzi, kuweka vipaumbele tofauti na Mungu mbele zaidi, kusema uongo na mambo mengine mengi.
*Ufunuo wa Yohana 5:10*
_*ukawafanya kuwa ufalme na makuhani kwa Mungu wetu; nao wanamiliki juu ya nchi.*_
Utagundua kwamba tuliponunuliwa alitufanya kuwa ufalme kwa maana ya kumiliki na makuhani kwa maana ya kupeleka ibada kwa Mungu wetu. Kuhani anasimamia ibada na mfalme anasimamia milki. Hivyo Yesu aliturudisha tena kwenye asili yetu ya kuumbwa kuabudu pamoja na kumiliki.
SEMINA YA NENO LA MUNGU RGCM DODOMA DAY 2️⃣
NAMNA YA KUENDEA MILKI ZAKO ULIZOAHIDIWA NA MUNGU NA ZILE ZILIZO KATIKA MIKONO YA ADUI.
Na Ev, Daniely Joshuan.
26th April 2024
Yesu alipokuja alikuja kurudisha nafasi hizi mbili.
Nafasi ya kifalme inayopeleka watu katika kumiliki.
Pili nafasi ya kikuhani inayompelekea mwanadamu kutoa ibada.
Mfalme wa kwanza ni Adamu na kuhani wa kwanza alikuwa Adamu. Na Yesu alipokuja alikuja kurudisha nafasi hizi mbili ambazo ni kanuni pacha. Shetani alichokifanya alikuja na kumyanganya Adamu nafasi yake na Mungu anapokuja anauliza huko wapi Adamu. Sasa Yesu alipokuja tuone alifanya nini?
Ufunuo wa Yohana 5:9-10
[9]Nao waimba wimbo mpya wakisema, Wastahili wewe kukitwaa hicho kitabu na kuzifungua muhuri zake; kwa kuwa ulichinjwa, ukamnunulia Mungu kwa damu yako watu wa kila kabila na lugha na jamaa na taifa, [10]ukawafanya kuwa ufalme na makuhani kwa Mungu wetu; nao wanamiliki juu ya nchi.
Unaona kile ambacho Yesu alikuja kufanya kwa kumwaga Damu yake. Anawarudisha watu ukuhani kwa maaana ya ibada na ufalme kwa maana ya utawala. Edeni ilitufanya kupoteza mambo haya makuu mawili na hivyo vivyo msalaba unarudisha nafasi hizi mbili UFALME na UKUHANI.
Yesu hakuja kuwafanya watu kuwa wakawaida, aliwaletea ufalme na ukuhani. Kwa namna ninavyofahamu mimi anayemjua Yesu Kristo anatakiwa kumiliki juu ya Nchi. Ungejua nini Mungu anasema kwenye neno lake unapomuamini usingekosa chakula. Kama kweli una Yesu lazima uwe mwanga na uwe chumvi. Siamini katika umasikini na kumtumikia Yesu katika ufukara. Hayupo mwanadamu aliyekuwa masikini kama Yesu lakini Biblia inasema alifanyika masikini ili kupitia huo tuweze kuwa matajiri.
Ufunuo wa Yohana 5:11-12
[11]Nikaona nikasikia sauti ya malaika wengi pande zote za kile kiti cha enzi, na za wale wenye uhai, na za wale wazee, na hesabu yao ilikuwa elfu kumi mara elfu kumi na elfu mara elfu, [12]wakisema kwa sauti kuu, Astahili Mwana-Kondoo aliyechinjwa, kuupokea uweza na utajiri na hekima na nguvu na heshima na utukufu na baraka.
Unaona namna Biblia inasema alichinjwa kupokea uweza na utajiri na hekima na nguvu na heshima na utukufu na baraka. Sijui kama uliookoka unajua kile ambacho ulipokea. Uweza hakwenda nao mbinguni aliuacha kwa kanisa. Na utajiri huu si wale wanaosema utajiri wa rohoni ni utajiri wa kuwa navyo vyote. Hekima hii mbinguni haina kazi ni kwa wale wa duniani kuweza kuwawezesha kumiliki na kutawala. There is no kingdom without Wisdom Kwa tafsiri isiyo rasmi ni kwamba hakuna ufalme bila hekima.
Heshima je una kiwango gani cha heshima wewe, sikatai kudharauliwa kuna madarasa hata mimi nimepita ya kudharauliwa lakini haikuwa milele. Jaribu likipitiliza muda wake linakuwa kifungo. Iko wapi heshima ya kanisa? Tumebeba mambo ya dini dini, na kanisa halijui kwamba ukristo siyo dini ni mahusiano. Utajua haya ukifika huko mbinguni pale ukishindwa kupokelewa maana huko hawapokei wanaokwenda kanisa bali wenye mahusiano na Kristo.
Anasema na Utukufu na baraka, kuna kiwango unafika kinakuwa na utukufu. Wafalme wanaelewa lugha ya utukufu. Baraka hizi ni kwa watu walioko duniani kwa sababu mbinguni hakuna kazi hiyo.
Ufunuo wa Yohana 5:13-14
[13]Na kila kiumbe kilichoko mbinguni na juu ya nchi na chini ya nchi ya juu ya bahari, na vitu vyote vilivyomo ndani yake, nalivisikia, vikisema, Baraka na heshima na utukufu na uweza una yeye aketiye juu ya kiti cha enzi, na yeye Mwana-Kondoo, hata milele na milele. [14]Na wale wenye uhai wanne wakasema, Amina. Na wale wazee wakaanguka, wakasujudu.
Unaona hapa na vitu vya baharini ikiwemo na yale majini yanayokupinga. Vitu vya chini ya bahari vilikiri na vya kwenye nchi vikakiri, hivyo ukisema nalima sipati majibu maana yake haujui kazi ya msalaba. Kama haujaelewa hivi vitu viwiki kwenye wokovu utajitaidi hautafika mwisho.
Tuliona jana shetani akimwambia Yesu milki zote hizi ukinisujudia nitakupa maana yake kuna ambao alishawapa baada ya wao kumpa ibada.
KANUNI ZA KUENDEA MILKI AMBAZO MUNGU AMEKUHAIDI
Kanuni ya Kwanza
Kurudi au kusimama tena katika ibada za kweli
Kitu ambacho kitakurudisha kwenye heshima, kwenye baraka ni kurudi na kusimama katika ibada za kweli. Hapa siongelei dini, wala misisimko ndani ya kanisa naongelea ibada ya kweli ambayo inamuhusu Mungu tu. Nikiandika na kukuhubiria namna hii nakuambia habari za mbulinguni. Wengi wanaona ibada njema kwa maana wamejibiwa matatizo yako.
Kanisa la sasa hivi alina ibada za kweli. Watu wa sasa hawana mpango wa kwenda mbinguni. Kila mtu anatafuta majibu ya maisha yake. Tunahitaji maabudu ya kweli ili sisi kurudi kwenye utawala wetu. Leo tuna watu wengi ambaobwako tayari kujipendekeza kwa wachungaji wao wakifikiria ni ibada sikiliza Mungu siyo muhuni.
Kuna kiwango cha maombi ambayo ni ibada, unaomba ili upone siyo vibaya lakini kuna ibada ambayo ni wewe na Mungu wako. Yesu anakutana na Msamaria na alikuwa mtu wa ibada ingawa alikuwa muhuni.
Yohana 4:20
Baba zetu waliabudu katika mlima huu, nanyi husema ya kwamba huko Yerusalemu ni mahali patupasapo kuabudia.
Huyu mama alikuwa mtu wa ibada na alikuwa na taratibu za ibada. Yesu alimwangalia huyu mama na akamwambia Lakini saa inakuja, nayo sasa ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli. Kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu. Yohana 4:23
Kama unaabudu na unaabudu usichokijua maisha yako hayawezi kuwa na badiliko. Utaona hapo chini namna anasema utafute kwanza ufalme wake na haki yake na mengine utazidishiwa utaelewa kile Yesu alikisema. Huyu mama alikuwa mtu wa ibada ingawa alikuwa na wanaume watano. Mtu yuko kanisani kwa miaka na anajiuliza mbona sipogi hatua sikiliza Mungu aliniambia leo nikiwa hotelini yeye hayuko radhi na watu wanaorahisisha. Ndiyo maana utakuwa na ndugu zako hawamuabudu Mungu na wanamaisha mazuri..lakini wewe huko ndani ya kanisa ni vuguvugu. Mungu hajawahi kukubaliana na warahisishaji.
Huyu mama alikuwa mtu wa kanisa na alijua mpaka mahali pa maabudu, lakini alikuwa mrahisishaji.
Kuna viwango viwili vya mwabudu halisi:-
1️⃣ Maabudu ya moyoni.
Moyo kuhusika katika ibada. Ibada yeyote unayotoa isitoke moyoni ni bure.
Mathayo 15:8
Watu hawa huniheshimu kwa midomo; Ila mioyo yao iko mbali nami.
Moja kati ya somo ambalo linapaswa kufundishwa sana kwenye kanisa la nyakati za mwisho ni somo la moyo. Moyo utahiriwe na kisu kipite na kukatakata na kutenga. Mungu aangalii bidii yako wala sura yako bali moyo wako. Moyo wako ni sura yako mbele za Mungu,
Watu wengi waliosema Mungu ameniona wengi wao hawamjui hata huyo Mungu. Mungu kukuona ni kama Esta aliyekuwa chokoraa alimtoa huko na kumpeleka kwenye kiti cha umalikia hiyi ndiyi kusema Mungu amemuona. Ni sawa na Daudi alitolewa mashambani alipokuwa anachunga porini na kuwa mfalme.
Mungu akikutana na wewe umri wako wala elimu yako haijalishi tena.
Ibada wa wengi hazitoki moyoni ndiyo maana hakuna matokeo wengi ni wanafiki. Unaweza kufanya ibada hata miaka kumi lakini kama umejaa mashindano, chuki, magomvi hakuna ibada hapo. Kuna mtu aliambiwa "Huna fungu wala huna sehemu katika jambo hili, kwa kuwa moyo wako si mnyofu mbele za Mungu." Matendo ya Mitume 8:21. Watu waakuja kanisani lakini mioyo yao siyo miyoofu na hawana fungu wala sehemu.
Kwenye ufalme wa shetani hakuna watu wanaigiza maana ukiigiza unakufa, ndiyo maana wako halisi sana kwa shetani. Lakini kanisani utawakuta watu waigizaji (pretenders). Kwenye ufalme wa shetani hakuna wanafiki maana utatoka na adhabu kwake. Tunao watu makanisani ni wanafiki na ndiyo maana mioyo yao haiko sawa na Mungu.
2️⃣ Mtindo wa Maisha yako
Nilifundisha kwamba mtindo wa maisha yako ndiyo shukurani yako naongeza kwa kusema mtindo wako wa maisha unaonyesha wewe unaabudu. Ikiwa unakuja kanisani na wewe ni kahaba maana yake mtindo wako wa maisha ndiyo maabudu yako.
Mwenye dhambi ni tafsiri ya mtu ambaye hawezi kujisaidia. Tulipokuwa wadhambi Yesu aliona kwamba hatuwezi kujisaidia ndiyo maana alikuja na kutusaidia. Ninaona wengine wanahubiri injili ya kuwalaumu wengine lakini wamesahau upendo wa Kristo aliyewajilia. Unapohubiri injili ya kuhukumu watu tu pekee wewe ni muongo.
Kama ukienda kanisani mtindo huo wa maisha yako ndiyo ibada, ukienda kuzini hayo ni maabudu yako.
Unajua hata kuavha dhambi ni shukurani pia.
Kanisa likitaka kuendea milki zake nimekuambia lazima lirudi mahali pa ibada ya kweli.
Sqali langu kwako unaishi maisha ya aina gani? Kwasababu ya kukosa hivi vitu viwili ibada zetu zimekosa kuabudu.
Yesu alifundisha kwa habari ya msamaria mwema.
Luka 10:30-32
[30]Yesu akajibu akasema, Mtu mmoja alishuka toka Yerusalemu kwenda Yeriko, akaangukia kati ya wanyang’anyi; wakamvua nguo, wakamtia jeraha, wakaenda zao, wakimwacha karibu ya kufa. [31]Kwa nasibu kuhani mmoja alishuka kwa njia ile; na alipomwona alipita kando. [32]Na Mlawi vivyo hivyo, alipofika pale akamwona, akapita kando.
Wakwanza kushuka alikuwa ni kuhani akampita kando na maandiko yanaongelea mlawi ambaye kwa kupindi kile walikuwa wachukua mafungu ya kumi na yeye alipita kando. Alipita msamaria mwema akamuona na alimuhurumia. Je? maisha yako yana huruma juu ya watu wengine.
Luka 10:34-35
[34]akakaribia, akamfunga jeraha zake, akizitia mafuta na divai; akampandisha juu ya mnyama wake, akampeleka mpaka nyumba ya wageni, akamtunza. [35]Hata siku ya pili akatoa dinari mbili, akampa mwenye nyumba ya wageni, akisema, Mtunze huyu, na cho chote utakachogharimiwa zaidi, mimi nitakaporudi nitakulipa.
Maisha yetu kama alama ya maabudu, kanisa limejaa wanafiki vile wanaabudu sivyo wanavyoishi. Siyo vibaya maana ndivyo nyakati za mwisho zinasema watu watajipenda wenyewe, watapenda fedha. Ndiyo maana wamejaa makanisani lakini maisha yao hayabadiliki.
Mungu utakayemuabudu ndiye Mungu ataleta uzito kwenye mifuko yako (The Lord you worship is the Lord will bring load in your wallet).
Maisha ya Ayubu ni mfano wa mtu aliyekuwa na ibada. Angalia sifa za Ayubu.
Ayubu 1:1-3
[1]Palikuwa na mtu katika nchi ya Usi, jina lake alikuwa akiitwa Ayubu; mtu huyo alikuwa mkamilifu na mwelekevu, ni mmoja aliyemcha Mungu, na kuepukana na uovu. [2]Kisha walizaliwa kwake wana saba, na binti watatu. [3]Mali yake nayo yalikuwa ni kondoo elfu saba, na ngamia elfu tatu, na jozi za ng’ombe mia tano, na punda wake mia tano, na watu wa nyumbani wengi sana; basi hivi mtu huyo alikuwa ni mkuu sana kuliko watu wote wa upande wa mashariki.
Kilichompa sifa zote hizi Ayubu ni nguvu ya kuabudu. Unaona maisha ya ibada ya Ayubu. Ukijua maisha ya ibada na kumcha Mungu na moyo mnyoofu Mungu uwa anaachilia mali. Mali si kitu cha kuchukua tu. Usipompa Mungu ibada inayostahili hakuna mahali utaenda. Kuwa mtu wa ibada ya kweli kama Ayubu ili uwe na mali. Kuna mtu anasema mbona kuna watu ambao hawana Mungu lakini wana vitu sikiliza nimekutana na watu walikuwa na vitu na hawakuwa na Mungu na sasa hawana Mungu.
Kama wewe ni mtu wa kuabudu hata kama wanakusema na kukusimanga usiache. Mungu si dhalimu shikamana na uaminifu wako mpaka mwisho.
Mungu hawasaidia wale warahisishaji, Ayubu alikuwa na mali kwasababu ya mambo manne yaliyotamkwa.
1️⃣Mkamilifu
2️⃣Mwelekevu
3️⃣Alimcha Mungu
4️⃣Alikuwa anaepuka uovu.
Kuna mtu unayesoma haya na Mungu anataka urudi kwenye msalaba na kumwambia Mungu nilipoteza Muda wangu na kufikiri kwamba naweza kufanikiwa.
Najua ulikuwa unafikiri haya ni mambo ya kupokea na kutabiriwa baraka. Umeshafanya hizo sarakasi za kutosha lakini umeenda wapi?. Nimekuja kukuonyesha kanuni za kibiblia ambazo zitakupeleka mahali.
Nimekuonyesha kanuni ya kwanza ya kuamua kuwa muabudu wa kweli. Kwa hivyo tuna watu ambao hawapandi viwango na wako ndani ya kanisa.
Kanuni ya Pili
Maombi
Zaburi 2:8
Uniombe, nami nitakupa mataifa kuwa urithi wako, Na miisho ya dunia kuwa milki yako.
Hii ni kanuni nyingine ya kufikia milki zako, nenda kaangalie Ibrahimu alikuwa mtu wa maombi, Yakobo alikuwa mtu wa maombi vivyo hivyo kwa Daudi alikuwa mtu wa maombi. Unajua Mungu anaposema uniombe siyo kwamba hajui unataka hapana ni kama vile anavyosema nikumbushe maana yake anakuita mahali pa maombi.
Hii ni siri ambayo amesema niombe nitakupa mataifa kuwa urithi wako siyo kijiji cha Bibi yako, anaongelea mataifa. Tunataka watu wafike mahali, si umesikia watu wanjenga dubai lakini wewe Goba tu inakushinda.
Je unajua maisha ya maombi, kuna aina ya maombi ambayo ukijiingiza lazima umiliki. Hakusema Dodoma wala singida amesema mataifa kuwa urithi wako.
Kesho nitakuonyesha aina ya maombi ambayo yatakuingiza kiurahisi kwenye miliki zako. Umekaa na mataifa mangapi ukajadili vitu vya maana ndipo useme nimeomba.