cover

DAY 4: EL- RACHUM

Ev Daniel • RGCM-GOBA • Apostolic Church •
ScripturesMithali 16:1

*Na Ev Daniely Joshuan*_ *04th September 2025* *NAMNA YA KUANDAA MOYO ILI KUTAFUTA REHEMA ZA MUNGU KWENYE KIWANGO CHA MSAMAHA* Hauwezi kukimbia kimbia kwamba Bwana ni samehe ni lazima ufundishwe namna ya kuandaa moyo ili kuzitafuta rehema za Mungu. Nakuomba usome na kusoma ili somo. Leo tutaangalia kitabu cha Mithali tu na kuna sababu kadhaa kwanini tunasoma mithali:- * Hiki ni kitabu kinachomfunua Yesu kama hekima ya Mungu. * Ni kitabu cha Mtu aliyeona rehema za Mungu (Suleimani). *Mithali 16:1* _*Maandalio ya moyo ni ya mwanadamu; Bali jawabu la ulimi hutoka kwa BWANA.*_ Huyu mtu Suleimani alikaa na akagundua kwamba:- * Mwanadamu anayo nafasi ya kuandaa moyo wake. Mwanadamu anawajibu wa kuandaa moyo wake ikiwa anataka kukutana na Mungu sasa haijalishi ni kwa baraka au kwa msamaha. Ndiyo maana tunajifunza namna ya kuandaa moyo kupata chochote kutoka kwa Mungu. Una wajibu wa kuandaa moyo wako. LAZIMA ujifunze au ufundishwe namna ya kuandaa moyo ni wajibu wako. Kama tunaweza kufanya tunachoweza kufanya Mungu anaweza kufanya TU kile anaweza kufanya. Hii habari ya wewe na Mungu kuna wajibu wako si kila kitu Mungu anafanya. Ni mara ngapi unaandaa moyo? Mkristo anaweza kuandaa nguo za jumapili lakini amesahau kuandaa moyo. Na ibada itakuwa kuingia na kutoka. Usijihudhurishe mbele za Mungu bila kuuandaa moyo wako ni kupoteza muda. * Mungu uitikia kwenye maadalizi yetu ya moyo zaidi ya maombi yetu. Mwitiko wa Mungu hauko katika mahitaji unayoleta bali katika maandalio ya moyo wako. Ndiyo maana anasema wenye moyo safi watamuona Mungu. *Mathayo 5:8* _*Heri wenye moyo safi; Maana hao watamwona Mungu.*_ Sasa nakufundisha kwenye eneo moja la msamaha lakini kuna eneo la baraka kuna aina ya maandalizi yake. Sara alicheka hakuamini baraka za Mungu na yalitokea kwasababu ya agano la Mungu na Ibrahimu. Maombi mengi hayajajipiwa kwasababu ya maandalizi ya moyo. Watu wengi wana hasara na wanashindwa kufika pale Mungu anapotaka kwasababu ya maandalizi ya mioyo yao. Barthomayo aliandaa moyo kutoka mbali hata walipomyamazisha bado alipiga kelele Yesu Mwana wa Daudi unirehemu. Zakayo aliandaa moyo na ndiyo maana Yesu alimkuta kwenye mkuyu. Niliwaambia watu mahali kwamba Roho ya uchungu ni alama ya kuzaa. Unapokuwa na uchungu unatoa muujiza wako kimakosa. Tatizo siyo tatizo ulilonalo tatizo ni moyo ulionao. Ndiyo maana matatizo mengi ya shetani yanaenda kushambulia moyo. Biblia inasema *Mithali 4:23* _*Linda moyo wako kuliko yote uyalindayo; Maana ndiko zitokako chemchemi za uzima.*_ Mtoto wa Mungu moyo ndiyo tatizo siyo ile shida uliyonayo. Sijajua kama unajua Mungu uwasukuma watu ili kuandaa mioyo yao. Niliwaambia watu mahali kwamba mikikimikiki ni jambo nzuri maana inaandaa na kutengeneza mioyo. Ni muhimu sana kujua kila tukio ambali unakutana nalo kwenye maisha yako linakufundisha nini? Hakuna mtu atatembea na Mungu kama moyo umeharibika. *Mithali 23:26* _*Mwanangu, nipe moyo wako; Macho yako yapendezwe na njia zangu.*_ Chukua maamuzi ya kuutoa moyo wako kuwa dhabihu na sadaka kwa Mungu. Suleimani anatufudisha haya na kile Mungu anataka kwetu. Kabla ya kunipa fedha, karama, magari nipe moyo. Je umefanikiwa kumpa Mungu moyo wako? Unaweza kumpa Mungu muda wako lakini si moyo wako. Suleimani anatufundisha Mungu anahitaji mioyo yetu. *Mithali 19:3* _*Upumbavu wa mtu hupotosha njia yake; Na moyo wake hununa juu ya BWANA.*_ Mtu hana maarifa ya kutosha juu ya Mungu hivyo anakutana na mambo magumu na kuanza kumnu'gunikia Mungu hana maarifa. Ndiyo maana nilisema utatembea na Mungu kwa *MAARIFA* na kwa *IMANI*. Wapumbavu wananuna kwasababu wamekataa maarifa ya Mungu. Haijalishi shetani anahusika kiasi gani lakini tambua kwamba Mungu anajua. Kuna watu wanamanuno! Hawataki huduma tena, hawataki kanisani tena, hawataki ndoa tena upumbavu wa moyo. *Mithali 3:3* _*Rehema na kweli zisifarakane nawe; Zifunge shingoni mwako; Ziandike juu ya kibao cha moyo wako.*_ Poteza kila kitu lakini usipoteze rehema za Mungu ndani ya moyo wako. Kila andiko ninalolitaja hakikisha unasoma na kuelewa maana kuna ujumbe ndani yake. *Mithali 18:12* _*Kabla ya uharibifu moyo wa mwanadamu hujivuna; Na kabla ya heshima hutangulia unyenyekevu.*_ Hakuna mtu anapewa heshima bila kunyenyekea. Na ukiona unapewa heshima bila kunyenyekea unaitwa uasi. Unataka kuinuliwa na kuwa na heshima chunga moyo wako usiharibike heshima ni matokeo ya kukubali kunyenyekea. Unakataa ushirikiano na watu wengine. Yesu mwenyewe pamoja na UUNGU wake alikuja na kuchagua wanadamu ambao walikuwa na mambo mengi na angeweza kuchagua malaika na kuwageuza wakamtii sana lakini alichagua wanadamu. Heshima ni matokeo ya kukubali kunyenyekea. *Mithali 4:23* _*Linda moyo wako kuliko yote uyalindayo; Maana ndiko zitokako chemchemi za uzima.*_ Huyu ni Suleimani mwenyewe anatuonyesha mwanadamu ndiye mlinzi wa kwanza wa moyo wake. Linda moyo wako uchungu usiingie, hasira isiingie majivuno yasiingie au aina yeyote ya mabaya. Anasema linda moyo wako kwanini hakusena nitakusaidia kulinda? Linda moyo wako kuliko magari, mke watoto au chochote ulichonacho. Wakati Ayubu anajaribiwa kilichokuwa cha kwanza moyoni au kile ambacho kilikuwa kipaumbele ndani ya moyo wake kilikuwa kinapigwa. Naomba nikuambie kitu hichi chochote ambacho utakipa kipaumbele cha kwanza ndani ya moyo wako Mungu atakitaka. Lakini jambo la pili chochote utakachoweka cha kwanza ndani ya moyo wako ni mng'ao kwa shetani. Acha kujiweka wazi kwenye ulimwengu wa Roho. Kumbuka ili kila mtu anapokujeruhi moyo wewe ndiye dhaifu siyo yeye. Uzima wa kila unachofanya uko ndani ya moyo wako. *Mithali 17:20* _*Mtu mwenye moyo wa ukaidi hatapata mema; Na mwenye ulimi wa upotofu huanguka katika misiba.*_ Watu wanahakisi maisha yao. Kwenye kiingereza anatumia moyo wenye hila. Kuna watu wanapita mahali pagumu kwasababu ya mioyo yao. Mapito ni mazuri kama utajitambua maana yanatengeneza mioyo lakini ni mabaya kama haujitambui maana yatageuza moyo. *Mithali 10:20* _*Ulimi wa mwenye haki ni kama fedha teule; Moyo wa mtu mbaya haufai kitu.*_ Mtu mwenye moyo mbaya hafai. Ni muhimu sana kuwa makini na watu wenye mioyo mibaya. Ni kwenye ndoa na n̈umegundua mtu hana moyo mbaya usinunue mapito. Kuna watu hawafai kwenye biashara kwasababu ya mioyo yao. Ndiyo maana Biblia inasema Yeremia 17:5 _*BWANA asema hivi, Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, Amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake Na moyoni mwake amemwacha BWANA.*_ Lazima ukatae moyo mgumu na moyo mbaya maana unakufanya usifae. *Mithali 19:21* _*Mna hila nyingi moyoni mwa mtu; Lakini shauri la BWANA ndilo litakalosimama.*_ Maana ya ili andiko ni kwamba hakuna mtu ambaye anaweza kushindana na Mungu akashinda. Panga ufanye unavyoweza lakini shauri la Bwana ndilo litasimama. Haijalishi wewe ni mbaya kiasi gani shauri la Mungu litasimama. Unaweza kujidanganya sana lakini nikuambie hakuna mtu mwenye uovu wa kutosha kwani shauri la Bwana ndilo litasimama. Ndiyo maana anasema *Isaya 33:1* _*Ole wako uharibuye ila hukuharibiwa, utendaye hila wala hukutendwa hila! Utakapokwisha kuharibu, utaharibiwa wewe; na utakapokwisha kutenda kwa hila, wao watakutenda hila wewe.*_ Hakuna moyo mwovu ambao umewahi kuharibu shauri la Mungu. Usiteswe na watu ambao wana mioyo miovu kwani shauri la Bwana ndilo litasimama. Wasikupe sonono kwani shauri la Bwana ndilo litasimama. Watanfanya hila... wafanye wafanyavyo lakini Mungu anakuandaa uwe na kiwango kingine. Mungu anajua namna ya kushughulika na mioyo miovu. *Mithali 11:20* _*Wenye kuhalifu moyoni ni chukizo kwa BWANA; Walio wakamilifu katika njia zao humpendeza.*_ Watu ambao ni wagumu kushugulika nao. Hawa ni watu wasumbufu na wahadahifu, ukiwaambia neno ili wakienda pande nyingine wanageuza. Hawa ni watu ambao hawasemesheki. Watu kama hawa hawafai ni chukizo kwa Bwana. Haiwezekani Bosi wako hana ujasiri wa kukusemesha wewe. Wewe hausimamii mambo jinsi yalivyo ni mtu mgumu kushugulikiwa. *Mithali 14:14* _*Ageukaye moyoni hushiba njia zake mwenyewe; Na mtu mwema ataridhika nafsini mwake.*_ Mageuko uanzia kwenye moyo. Mithali 16:5 _*Kila mwenye moyo wa kiburi ni chukizo kwa BWANA; Hakika, hatakosa adhabu.*_ Biblia ya kiingereza inasema hata kama utajiunga na watu hautakosa adhabu. Watu wenye moyo wa kiburi ni watu wanaopenda makundi. Mungu amesema hawatakosa adhabu. Ni neema ilioje kuyajua haya kabla ya kupata mabaya. Nimejenga tu msingi wa kuonyesha hekima ya Mungu juu ya mioyo ya wanadamu. Rehema za Mungu zinaposhushwa kwako unajielewa? Nataka siku ya leo mwambie Bwana nirehemu mabaya yote niliyopigwa kwayo kwasababu ya moyo wa kiburi nirehemu......omba sasa. *Restoration Gospel Commission Ministry,* *P.O.Box 32520,* *Goba Centre, Dar es salaam, Tanzania,* *Email: info@rgcm.org,* *Contact: +255 764 711 544,* *Web: https://www.rgcm.org.*

Comments

No comments yet.

Please login to comment.